Jumanne 2 Desemba 2025 - 08:00
Jenerali mstaafu wa Israel: Jeshi Linakabiliwa na Mgogoro Mkubwa Zaidi wa Rasilimali Watu Katika Historia Yake

Hawza/ Ya‘qub Brick, katika makala iliyochapishwa kwenye gazeti la Kizayuni la Maariv, ametangaza kwamba katika miezi ya hivi karibuni maelfu ya maafisa na sajenti wamekataa kuendelea na huduma yao ya kijeshi.

Kwa mujibu wa ripoti ya huduma ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ya‘qub Brick, jenerali mstaafu wa Israel, amesema kuwa baadhi ya watu kwa “visingizio mbalimbali” wanakataa kutekeleza wajibu wao, na wengine pia wamekataa kuongeza muda wa huduma yao ya kijeshi. Ameongeza kuwa; idadi kubwa ya maafisa wamewasilisha mara moja maombi ya kuachishwa kazi, na askari vijana pia hawako tayari kusaini mikataba ya huduma ya kudumu.

Amesisitiza kuwa mwenendo huu umesababisha “upungufu mkubwa wa nguvu kazi ya kitaaluma” ndani ya jeshi.

Brick, akirejea kwamba kupungua kwa kasi kwa idadi ya askari kumeathiri matengenezo ya vifaa vya kijeshi na utendaji wa mifumo ya mapambano, alionya kuwa kuendelea kwa hali hii kunaweza “kulilemaza kabisa jeshi katika muda mfupi”.

Jenerali huyo mstaafu aliwatuhumu Wakuu wa Majeshi wa miaka ya hivi karibuni kwa kuchukua “maamuzi yasiyofaa”, na kusema kuwa hatua kama “kupunguzwa kwa kiwango kikubwa cha askari” na kupunguza muda wa huduma ya kijeshi hadi miaka 3 kwa wanaume na miaka 2 kwa wanawake, kumeacha mianya ambayo haiwezi kuzibwa upesi.

Brick amebainisha kuwa; sera hizi zimesababisha askari wengi waliokuwa wa kitaaluma na wenye uzoefu mkubwa kuondoka jeshini, na badala yake katika nafasi nyeti kubaki watu ambao hawana uwezo wa kukabiliana na ugumu wa mazingira ya sasa ya vita.

Akiikosoa idara ya rasilimali watu ya jeshi, alisema idara hiyo kwa miaka mingi imekuwa ikifanya kazi bila taaluma na bila uwajibikaji, na matatizo ya msingi katika upangaji wa rasilimali watu yamepuuzwa. Kwa mujibu wa Brick, jeshi kutokana na matumizi ya mifumo ya teknolojia ya zamani na hifadhidata zilizotawanyika, limejikuta katika ombwe la taarifa.

Brick alitoa tena onyo kwamba mgogoro wa nguvu kazi unaweza kupoozesha kabisa operesheni za jeshi la Israel.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, katika mashambulizi ya miaka miwili ya jeshi la Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza, wanajeshi 923 wa Israel wameuawa na watu 6,399 wamejeruhiwa. Vyombo vya habari vya Israel pia vimeripoti kuwa takriban wanajeshi 20,000 wamepata msongo wa mawazo baada ya tukio la mshtuko (PTSD).

Katika ripoti hizo pia imeelezwa kuwa; Israel kutokana na udhibiti mkali wa kijeshi na hofu kuhusu hali ya kisaikolojia ya umma, inatuhumiwa kuficha takwimu halisi za vifo vyake.

Israel, kwa msaada wa Marekani, kuanzia tarehe 8 Oktoba 2023 ilianzisha mashambulizi ya miaka miwili dhidi ya Ukanda wa Ghaza, ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 70,000 na kujeruhi watu 170,000 — wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Mashambulizi haya yamesababisha uharibifu mkubwa, na Umoja wa Mataifa umekadiria gharama ya ujenzi mpya kuwa takriban dola bilioni 70.

Chanzo: Anadolu Ajansı

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha